Powered By Blogger

Friday, November 9, 2018

WABUNGE WACHARUKA KUHUSU MISHAHARA




SIKU tatu baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuwasilisha bungeni Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Mwaka 2019/2020 na kueleza ongezeko la mishahara ya wafanyakazi, Bunge limechachamaa na kuitaka serikali itoe kauli ya kina juu ya hilo.
Hatua hiyo imedaiwa na Bunge kuwa inatokana na kitendo cha serikali, kutopandisha mishahara hiyo kwa muda wa miaka mitatu sasa, jambo ambalo limesema halikubaliki na halivumiliki tena.
Spika wa Bunge, Job Ndugai, jana aliungana na wabunge wa pande zote mbili kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ambao bila kujali itikadi zao za kisiasa, waliibana serikali wakitaka itoe kauli ya kina juu ya upandishaji wa mishahara ya wafanyakazi.
Jumanne wiki hii wakati akiwasilisha mpango huo, Dk Mpango alisema katika kipindi cha muda wa kati yaani 2019/2020 na 2021/2022, mishahara ya wafanyakazi, wakiwamo wa taasisi za umma itaongezeka.
“Katika kipindi cha mwaka 2019/2020, mishahara ikijumuisha mishahara ya taasisi inakadiriwa kuwa Sh bilioni 7,559.0 na kukadiriwa kuongezeka hadi shilingi bilioni 8,422.7 mwaka 2021/2022,” Dk Mpango aliliambia Bunge.
Hata hivyo, Spika Ndugai alisema suala la kupandishwa kwa mishahara ya wafanyakazi ni suala nyeti na aliitaka serikali kulitolea kauli ya kina, akisema linalalamikiwa katika kila kona ya nchi.
Alisema pamoja na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na serikali, lakini upo uzembe unaofanywa na baadhi ya watendaji wa serikali katika kushughulikia maslahi ya watumishi, ikiwemo mishahara, upandishaji madaraja na ulipaji wa posho mbalimbali. Aliitaka serikali kuwasilisha bungeni kauli yenye takwimu na uhalisia kuhusu masuala hayo Alhamisi wiki ijayo.
Alisema kitendo cha serikali kushindwa kupandisha mishahara ya wafanyakazi kwa muda wa miaka mitatu, kinasababisha manung’uniko mengi ya watumishi na kutia doa uendeshaji wa serikali.
“Mtumishi anakaa miaka kumi bila kupanda cheo na hata anapopanda hapandi kwa mserereko kama inavyotakiwa, suala hili sisi kama Bunge hatuwezi kuendelea kuona linatokea… ni lazima serikali ilete majibu ya uhakika hapa,” alisema Spika Ndugai.
Awali, Mbunge wa Muheza, Balozi Adadi Rajabu (CCM) akichangia mpango huo, alisema suala la kutopanda kwa mishahara ya wafanyakazi wa umma kwa miaka mitatu, linatia doa tija na ufanisi katika maeneo mengi ya kazi.
“Mheshimiwa Waziri wa Fedha (Dk Mpango) nakuomba sana hili suala la mishahara ya watumishi wa umma lishughulikiwe haraka na serikali itoe kauli haraka ili kurudisha motisha ya wafanyakazi inayozidi kushuka siku hadi siku,” alisema Balozi Adadi.
Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe (Chadema) alisema iwapo serikali inataka kufikia tija katika miradi mikubwa inayoitekeleza, ni lazima katika bajeti ijayo ipandishe mishahara kwa kiwango ambacho kitafuta machungu waliyonayo wafanyakazi hivi sasa kutokana na kutopanda kwa mishahara kwa miaka mitatu.

No comments:

Post a Comment